Breaking News

WATOTO 92,698 KUPATIWA CHANJO YA POLIO NYAMAGANA MKOANI MWANZA

 Na Tonny Alphonce, Mwanza.

Watoto zaidi ya 92,698 wenye umri wa chini ya miaka mitano wa wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone ya ugonjwa wa Polio ikiwa ni jitihada za Serikali kuutokomeza ugonjwa huo ambao husababisha ulemavu wa kudumu kwa mtoto.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bibi Amina Makilagi akifungua rasimi kampeni ya chanjo kwa wilaya ya Nyamagana.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo kwa wilaya ya Nyamagana uliofanyika leo tarehe 18/05/2022 katika kata ya Mkolani,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bibi Amina Makilagi amesema ili kufanikisha zoezi hilo wataalamu watapita katika makazi ya watu,sehemu zenye mikusanyiko na katika maeneo ya ibada ili kila mtoto aweze kupatiwa chanjo hiyo.

Bi. Makilagi amesema maamuzi ya kuwafata wazazi na walezi kule walipo itawapunguzia Wazazi umbali wa kupata huduma hiyo lakini pia itawasaidia wataalamu kujua idadi kamili ya watoto watakaopatiwa chanjo kwa wilaya ya Nyamagana.

“Kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika mkoa wetu wa Mwanza ambao wanatoka nchi za jirani kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi hivyo wazazi lazima mkubali watoto waweze kupata chanjo vinginevyo watoto wetu watapata ulemavu na mimi nimewahi kuwaona wazazi waliokaidi kuwachanja Watoto wao baada ya miaka michache kupita wakapata ulemavu.”alisema Bi Makilagi.

Amesema ugonjwa wa Polio unaambukizwa na kirusi kiitwacho Polio,ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yoyote katika umri wowote ila kundi la watoto huathirika zaidi kutokana na kinga zao kuwa chini.


Bi. Makilagi mesema kirusi hiki kinaweza kuingia mwilini kupitia kwenye chakula,Maji au vitu mbalimbali ambavyo vimechafuliwa na virusi hivyo ambavyo vikiingia mwilini hukaa kwenye utumbo na kuanza kuzaliana na mwisho husababisha ulemavu.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa jiji la Mwanza Daktari Sebastian Pima amesema hamasa ya wazazi ni kubwa tofauti na chanjo zingine kwa kuwa wazazi wengi wamejitokeza kwaajili ya kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo.

Mganga Mkuu wa jiji la Mwanza Daktari Sebastian Pima akiongea na wanahabari hawapo pichani kuhusu namna zoezi la chanjo litakavyofanyika.

Daktari Pima amesema chanjo hii ya Polio itatolewa kwa siku 4 kuanzia leo tarehe 18/05/2022 hadi tarehe 21/05/2025 ambapo wazazi wanaweza kuwapeleka watoto wao katika vituo vilivyoainishwa pamoja na kwenye vituo vya afya vilivyo karibu nao.

Mzazi Zena Zuberi mkazi wa kata ya Mkolani Jijini Mwanza,amesema chanjo ya Polio haina shida kwa kuwa anaijua na watoto wake wote wamewahi kuchanjwa na hawakupata matatizo yoyote hadi wamekua watu wazima hivi sasa.


Zena Zuberi mkazi wa kata ya Mkolani Jijini Mwanza akielezea manufaa ya chanjo ya Polio kwa watoto wadogo

“Bado wengine wanatuambia hawataki watoto wao wachanjwe lakini hii chanjo ni ya kawaida hadi sasa mimi sijui kwa nini hawataki kuchanja wakati karibia watanzania wote tumechanjwa chanjo ya Polio”alisema Zena.

Nae Tunda Sabi au mama Hamisi amesema ameamua kumpeleka mtoto wake akapate chanjo kwa kuwa ni haki yake ya msingi lakini pia ni maelekezo ya Serikali hivyo hana budi kutekeleza zoezi hilo ambalo limeanza wilayani Nyamagana.

Tunda Sabi mzazi aliyejitokeza katika kampeni ya utoaji chanjo ya Polio kwa watoto akizungumzia namna zoezi lilivyofanyika.

Mama Hamisi amewaka wazazi kuwapeleka watoto wakapatiwe chanjo kwa kuwa mtoto asipopata chanjo hii ni wazi familia ndio itakayoathirika endapo mtoto atapata ulemavu wa kudumu utakao sababishwa na kirusi Polio.

Hatua hii ya kampeni ya chanjo kwa mkoa wa Mwanza inafanyika wakati nchi ya Malawi ikiwa imeshambuliwa na mlipuko wa ugonjwa huo kuanzia February 17 mwaka huu baada ya mtoto mmoja  kutoka mji mkuu wa Lilongwe kudhibitika kuwa na ugonjwa huo.

Kuanza kwa kampeni hii mkoani Mwanza itasaidia kuzuia ugonjwa huo wa Polio usiingie nchini na hasa mkoani Mwanza kwa kuwa kuna mwingiliano wa kibiashara na huduma kutoka nchini Malawi.


Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni ya utoaji chanjo kwa wilaya ya Nyamagana.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya mara ya mwisho Tanzania ilipata ugonjwa wa Polio mwaka 1996.

Kampeni hii ya chanjo ni utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 1990 ambayo inatoa kipaumbele katika utoaji huduma za kinga, tiba,uhamasishaji na utengano ambapo huduma hizi hutolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Katika utoaji huduma hizo,msisitizo umeelekezwa katika utoaji wa chanjo, elimu ya afya na kuruhusu upatikanaji wa huduma hizo bila malipo.

Taarifa ya hali ya Malezi Jumuishi nchini Tanzania inaonyesha uwekezaji wa Serikali katika uhai wa mtoto unaonekana dhahiri kupungua  kwa vifo vya watoto kati ya mwaka 2010 na 2015.  


Credit:Nicolas Kajoba (picha ya matone)      

No comments