Breaking News

EMEDO YAIOMBA SERIKALI KUONDOA USHURU WA VIFAA VYA UOKOAJI MAJINI ILI KUNUSURU MAISHA YA WAVUVI


Na Tonny Alphonce,Mwanza

Serikali imeombwa kuondoa ushuru kwa bidhaa za uokoaji majini ili kutoa nafasi kwa wavuvi na wasafiri wa majini kununua bidhaa hizo kwa bei ya kawaida.

Mratibu wa mradi wa kupunguza ajali za kuzama majini Arthur Mugema wakati akiongea na waandishi wa habari.

Ushauri huo umetolewa na mratibu wa mradi wa kupunguza ajali za kuzama majini wa shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo Tanzania (EMEDO) Arthur Mugema wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.

Arthur amesema kutokana na vifaa vya kuzuia kuzama watu majini zikiwemo Jaketi maalumu kuwa bei ghali wavuvi wengi hukimbilia kununua Jaketi za bei nafuu ambapo ajali ikitokea Mvuvi anaweza kuzama na kufa maji kutokana na Jaketi aliyonayo kutokuwa na ubora unaotakiwa.

Amesema kutokana na kipato cha wavuvi kutokuwa kikubwa ni vema Serikali ikaangalia uwezekano wa kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vyote vya usalama vinavyotumika majini ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaofanya shughuli zao za kiuchumi majini.


Arthur amesema Jaketi lenye ubora na usalama linauzwa kuanzia shilingi 40,000 hadi 50,000 kiasi ambacho ni kikubwa kiasi kwamba Wavuvi wadogo hawawezi kumudu gharama hiyo.

“Ukiachilia mbali Imani za kishirikina za kukataa kuvaa majaketi ya kuwazuia kuzama lakini na bei nayo ni kikwazo kikubwa  hivyo wavuvi wengi huamua kutovaa na matokeo yake ajali inapotokea wengi wao hufariki dunia.”alisema Arthur.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mtendaji wa EMEDO Editrudith Lukanga amesema katika kuhakikisha jitihada zinachukuliwa za kupunguza vifo vya majini tayari shirika la EMEDO kwa kushirikiana na Taasisi kutoka Wingereza inayohusika na masuala ya usalama kwenye maji na uokoaji RNLI wameingia mkataba wa miaka mitatu wa kusaidia jamii za wavuvi.


Mkurugenzi  Mtendaji wa EMEDO Editrudith Lukanga akiongea na wanahabari hawapo pichani.

“Eneo hili la ajali za majini limesahaulika kiukweli mara nyingi tumekuwa tukisikia au kuona elimu ya usalama barabarani inatolewa au takwimu za ajali za barabarani zikitolewa lakini ajali za majini huoni jitihada kubwa zikichukuliwa kuhakikisha ajali hizo hazitokei”.alisema Bi Lukanga

Amesema Mradi huu ni wa kwanza kutekelezwa Ziwa Victoria na Unagharimu shilingi Bilioni 2.7 na  unatekelekelezwa kwa miaka mitatu ukilenga kupunguza hatari za kuzama majini kwa jamii ya Wavuvi waliko mikoa ya Mwanza,Kagera  na Mara.

“Tayari tumeanza kutekeleza mradi huu na vijana wetu tayari wapo kazini ambapo wengine wapo mkoani Kagera kwa sasa na tunaendelea kutekeleza mradi huu tukishirikiana na serikali.”alisema Bi Lukanga.

Wavuvi laki moja wanaofanya shughuli zao na kuishi pembezoni mwa  Ziwa Victoria ,Mia mbili Thelathini na Moja, kati yao  wanapoteza maisha kwa mwaka kwa kuzama majini.

Shirika la EMEDO ni miongoni mwa wadhamini wa Usiku wa Waandishi wa habari na Wadau wa habari unaoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza utakaofanyika Mwanza tarehe 03/06/2022 katika ukumbi wa Rock City Mall.

No comments