Breaking News

RC MAKALLA AZINDUA MIUNDOMBINU YA ELIMU MRADI WA BOOST ILEMELA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla ameupongeza uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati Miradi ya Maendeleo ikiwemo Miundombinu ya Shule za Awali na Msingi inayotekelezwa na BOOST kwa zaidi ya Bilioni 1.56.

Makalla ametoa pongezi hizo leo Septemba 13, 2023 katika hafla ya Makabidhiano ya Miundombinu ya Shule za Awali na Msingi zilizotekelezwa kupitia Mradi wa BOOST iliyofanyika kwenye Shule Mpya ya Buteja ambapo amesema uboreshaji huo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

"Mkoa wa Mwanza kupitia mradi wa BOOST tumepokea zaidi ya Bilioni 12 kwenye Kuboresha Miundombinu ya Elimu ya Msingi, kwakweli huyu Rais ana upenddo yaani kila kukicha anamwaga fedha kwenye miradi kedekede kwa Watanzania." Mkuu wa Mkoa.

"Leo nimefarijika maana katika Mkoa wa Mwanza Ilemela mmekua wa Kwanza kukabidhi Miradi ya Elimu ya BOOST na nitumie wasaa huu kuwahsukuru viongozi wote wa wilaya hii wa chama na Serikali kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kusimamia ujenzi wa Miundombinu hii kwakweli mmefanya kazi nzuri sana." Makalla.

Halikadhalika, ametumia wasaa huo kukemea tabia ya utoro wa wanafunzi na amewaagiza wazazi kusimama kidete kuhakikisha watoto wanapata elimu bila kukatisha na pia akakemea tabia ya kuozesha watoto kwa Tamaa ya kupata fedha kupitia mahari kwani wanakatisha ndoto za watoto.

"Ndugu wazazi nawaomba muitikie wito wa kuhakikisha watoto wetu wanapata Chakula wawapo shuleni kwani kinasaidia kuongeza ufaulu na nimewaagiza kuwepo kwa bodies Hai za shule ili kuleta ufanisi wa huduma lakini ninyi wazazi na walezi tambueni kuwa mna wajibu wa kushirikiana na juhudi hizo."

Mkuu wa Wilaya ya Ilemema Mhe. Hassan Masala amebainisha kuwa ukamilishaji wa Miradi hiyo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani kwa uwiano unaofaa kuketi kwenye viti Meza na kwamba wamekubaliana kuanza kutumia rasmi Miundombinu hiyo mara tu shule zitapofunguliwa wiki ijayo.

Adv. Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amesema vyumba 54 vya Madarasa,  vyoo matundu 70, majengo 2 ya Utawala, Ofisi ya Mwalimu, Madawati 1075, Viti 90 na Meza 90 vya elimu ya awali, Viti 74 na Meza 74 za walimu pamoja na Miundombinu ya viwanja vya michezo vimegharimu zaidi ya Tshs. 1.56 za mradi wa BOOST.

Kibamba amesema Ujenzi wa Miundombinu hiyo yote utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuendlea kuboresha huduma za jamii ambazo zimekua zikisaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi.

Aidha, amebainisha kuwa usimamizi wa pamoja wa kina baina ya viongozi wa Wilaya hiyo umesaidia kukamilisha kwa wakati kwa ujenzi ulioanza Mei Mosi mwaka huu na Kukamilia Agosti 30 na ametoa shukrani kwa wananchi waliochangia nguvu kazi za zaidi ya Milioni 500 kwenye ujenzi huo.





No comments