Breaking News

THRDC YAWANOA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU UANDISHI WA RIPOTI ZA MASUALA YA HAKI ZA BINADAMU

 


Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) umeendesha mafunzo ya siku mbili kwa watetezi wa haki za binadamu takribani 25 nchini,mafunzo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo watetezi hao wa haki za bianamu juu ya ufuatiliaji,utunzaji wa kumbukumbu na uandishi wa ripoti za masuala ya haki za binadamu,yaliyofanyika Bunju mkoani Dar es salaam.

Mafunzo hayo yaliyoanza hapo jana Agosti 5,2021 yatahitimishwa hii leo Agosti 6,2021 ambapo washiriki wa mafunzo hayo wamejengewa uwezo juu ya masuala mbalimbali ikiwemo namna ya uandishi wa ripoti zenye ubora.

Wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo hapo jana Meneja Programu kutoka THRDC,Remmy Lema amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwakumbusha watetezi wa haki za binadamu kuhusu masuala ya uandishi wa ripoti na kuweka mikakati ya kuona namna gani ya kufanya kwa ubora zaidi.

Ameongeza mara nyingi watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakijikita katika matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ingawa kuna maeneo mengi katika sekta mbalimbali ambazo wanaweza kufanya ufuatiliaji akitolea mfano sekta ya elimu,maji na afya,pia amewaasa washiriki kuchukua tahadhari zote za kujikinga na maambukizi vya virusi vya uviko-19 ikiwemo kuvaa barakoa, kuzingatia umbali kati ya mtu mmoja na mwingine wakati wote wa mafunzo hayo.

Naye Wakili kutoka THRDC, Leopold Mosha (Head of Protection Programs) wakati akiwasilisha mada katika mafunzo hayo amewaasa washiriki kuzingatia misingi ya kisheria wakati wa uandishi wa ripoti hizo na pia kuhakikisha wanajumuisha pande zote ikiwemo vyanzo vya mamlaka ili ripoti zao zisiwe na ombwe.

Wakili Mosha ameongeza kuwa kama watetezi wa haki za binadamu lazima wawe na ufahamu wa kisheria ili wakati wa uandishi wa ripoti zao waweze kufahamu ni za mlengo gani.

Pia amewaelekeza washiriki hao jinsi gani wanaweza kufanya mahojiano na vyanzo mbalimbali vya taarifa wakati wa ukusanyaji wa taarifa za matukio ya haki za binadamu.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa THRDC,Onesmo Olengurumwa alipata nafasi ya kuwafundisha wanshiriki kuhusu kanuni za uandishi na namna bora ya kuandika ripoti za haki za binadamu .Baadi ya mambo muhimu ni pamoja na namna ya kuandika Kichwa cha ripoti  hakipaswi kuonyesha kuegemea upande wowote, mpangilio wa ripoti, uchaguzi wa picha zenye ubora, michoro pamoja na kuweka takwimu kunaongeza uzito wa ripoti hiyo.

“Ukiwa unafanya haya niliyokuelekeza utakuwa mtetezi ambaye anafanya vitu vyake na vinaonekana” amesema Olengurumwa wakati akiwasilisha mada kuhusu Ripoti za haki za binadamu na kuongeza kuwa mara nyingi ripoti huandikwa na mtu mmoja na kama kuna ulazima wa kuandikwa na watu wengi wanapaswa kugawana kurasa za kuandika na baadaye kuunganishwa na kupata ripoti kamili.

Pia amesema ili kupata ripoti kamili kuhusiana na maswala ya haki za kibinadamu lazima kuwe na uchambuzi wa kisheria, ukweli na jinsia husika, na kuwataka washiriki hao wakati wanaadika ripoti zao ni lazima wawe na taarifa zenye ukweli pamoja na kufahamu lengo na walengwa wa ripoti hiyo ili waweze kuiandika kwa ubora Zaidi.

Olengurumwa amesisitiza ¬¬¬ kuwa ripoti bora lazima iwe na hitimisho pamoja na maoni ya nini kifanyike ili kutatua tatizo hilo na pia Kichwa cha ripoti hiyo hakipaswi kuonyesha kuegema upande mmoja.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru THRDC kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo kuhusu masuala kadhaa wakati wa uandaaji wa ripoti za masuala ya haki za binadamu ikiwemo namna ya kufanya mahojiano wakati wa kukusanya taarifa za matukio mbali mbali za matukio ya haki za binadamu.

“Ninaishukuru sana THRDC kwa kuandaa mafunzo haya nimejifunza mengi kuhusu uandaaji wa ripoti na nitakwenda kuyafanyia kazi katika shirika langu pamoja na kufanya ufuatiliaji wa kazi tunazozifanya,”amesema John Myola mmoja wa washiriki wa mafunzo.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania tangu kuanzishwa kwake umekuwa ukiandaa semina,mafunzo na warsha mbalimbali ambazo zinalenga kuwajengea uwezo wanachama wa mtandao huo na wada mbalimbali kuhusu masuala kadha wa kadha  yahusuyo na hivi karibuni mnamo Julai mosi mwaka huu THRDC iliwajengea uwezo wanachama wake takribani 70 kuhusu masuala ya kodi warsha ambayo ilihudhuriwa na wadau na viongozi  mbalimbali akiwemo  Afisa Mkuu wa Kodi  kutoka TRA na Meneja TRA Kinondoni.


Watetezi TV

Dar es salaam

6/08/2021

No comments