Breaking News

WANAFUNZI WAONDOKANA KUSOMA SHULE UMBALI MREFU, BAADA YA KUJENGWA SHULE MPYA YA SEKONDARI

 

Na Marco Maduhu, SHINYANGA


WANAFUNZI ambao ni wakazi wa Mega Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wameondokana na changamoto ya kwenda kusoma shule umbali mrefu, mara baada ya kujengwa shule mpya ya Sekondari eneo hilo.

Mkuu wa shule hiyo mpya Mega Sekondari, Revocatus Masembo, alibainisha hayo juzi wakati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Philemon Sengati, alipofanya ziara ya kukagua màendeleo ya shule hiyo, akiwa na wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa.

Alisema kujengwa kwa shule hiyo, kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapunguza adha wanafunzi kwenda kufuata masomo umbali mrefu, katika Kata jirani ya Segese umbali wa Kilomita Nane, na kusababisha baadhi yao kukatisha masomo ikiwamo kupewa ujauzito.

"Shule hii mpya ya Sekondari Mega, imeanza kutoa elimu mwaka huu, na tunajumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 82, wasichana 56, wavulana 26, na vyumba vya madarasa vipo vinne, pamoja na maabara za Sayansi kwa ajili ya wanafunzi kusoma kwa vitendo," alisema Masembo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, alisema Serikali ilianzisha ujenzi wa Shule hiyo mpya, kwa kushirikiana na nguvu za wananchi, mara baada ya kuona wanafunzi wanateseka kufuata masomo umbali mrefu, ndipo ikabidi waitatue changamoto hiyo ili watimize ndoto zao.

Aidha, alisema suala la ukosefu huduma ya umeme na maji kwenye shule hiyo atalishughulikia, ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri, na kupata elimu bora.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, alisema ujenzi wa shule hiyo ni utekelezaji wa ilani ya chama hicho, kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu katika mazingira rafiki.

No comments