Breaking News

OFISI YA MBUNGE NYAMAGANA YAPONGEZWA KUWAKUMBUKA WATOTO WENYE ULEMAVU.

 

Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Shule ya msingi Buhongwa iliyoko wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza imeishukuru ofisi ya mbunge jimbo la Nyamagana kwa kutoa fedha za ujenzi wa matundu kumi ya Choo utakayozingatia  uwepo wa  wanafunzi wenye ulemavu shuleni hapo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Buhongwa Oliver Benedicto akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa matundu 10 ya Choo katika shule ya Buhongwa Mwanza.

Akizungumza mbele ya kamati ya mfuko wa jimbo la Nyamagana jiji la Mwanza Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Buhongwa Oliver Benedicto amesema msaada huo wa ujenzi wa mashimo 10 ya choo utamaliza tatizo la msongamano wa wanafunzi Chooni.

Mwalimu Oliver amesema shule ya msingi Buhongwa inakitengo cha wanafunzi wenye ulemavu na wale wenye mahitaji maalumu hivyo kukamilika kwa Choo hicho kutasaidia wanafunzi kujisaidia bila tatizo lolote kutokana na miundombinu kuwa rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu.

“Kiukweli tunamshukuru sana Mh Mbunge Stanslaus Mabula kwa kutupatia sh.milioni 5 kwaajili ya ujenzi wa Choo hiki ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 70 na bahati mbaya fedha zimeisha na tunamuomba Mbunge au wadau wengine watupatie kama milioni 4 ili tukamishe ujenzi wa Choo hiki”.alisema Mwl Oliver.

Akizungumzia faida watakazozipata wanafunzi mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Choo hicho,Mwl Oliver amesema kutapunguza uhaba matundu ya Vyoo kwa wanafunzi wa kawaida na wale wenye ulemavu,kutafanya watoto wawe kwenye mazingira salama ya kujistiri na kutaimalisha afya za wanafunzi kwa kujisaidia katika mazingira safi hasa kwa upande wa wanafunzi wenye ulemavu wa madarasa ya awali.

Akizungumzia miundo mbinu ya shule ya msingi Buhongwa kwa wanafunzi wenye ulemavu Mwl Mkuu Oliver Benedicto amesema mazingira awali hayakuwa rafiki na shule imeanza kubadili miundombinu taratibu kila inapoongeza majengo mapya ili yaweze kutumiwa pia na wanafunzi wenye ulemavu.

“Serikali imeliona matatizo wanayopata wanafunzi wenye ulemavu na ndio maana majengo ya zamani tumeyaongezea ngazi zitakazowawezesha hata wanafunzi wenye ulemavu waweze kuyatumia na kwa majengo mapya kipaumbele chetu ni kuweka mazingira mazuri pia kwa Watoto wenye ulemavu”,alisema Mwl Oliver

Kwa upande wa taaluma kwa wanafunzi wenye ulemavu na wale wa mahitaji maalumu Mwl Oliver amesema shule yake bado inauhitaji wa walimu kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kuwa waliopo hawatoshi.

Mjumbe wa mfuko wa jimbo la Nyamagana jiji la Mwanza Ramadhani Salum amempongeza Mwl mkuu wa shule msingi Buhongwa kwa kutumia vizuri fedha za mfuko wa bunge zilizotolewa na mh mbunge na kuahidi kulifikisha kwa mbunge ombi la shule hiyo la milioni 4 ili kukalmilisha ujenzi wa Choo hicho.

Mjumbe wa mfuko wa jimbo la Nyamagana jiji la Mwanza Ramadhani Salum akielezea kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa matundu 10 ya Choo katika shule ya msingi Buhongwa Mwanza.

Jovither Mwombeki mratibu wa lishe mkoa idara ya Elimu amesema wao kama mkoa kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu kuanzia wa darasa la awali wanakuwa na mazingira rafiki ya kusomea sambamba na kusimamia ujenzi wowote mpya uzingatie usawa kwa wanafunzi wote.

Akizungumzia kauli mbiu ya Siku ya Walemavu ya mwaka huu inayosema Si kila ulemavu unaonekana Jovither amesema ni jukumu la walimu kuwa makini wanapowafundisha Watoto na kujitahidi kuwanao karibu ili kujua mapungufu yao kwa kuwa kuna wanafunzi wanaweza kuwa na ulemavu uliojificha.

No comments